HABIBA ZARALI-PEMBA
Mti unapoanguka msituni, wengi husikia kishindo chake, Lakini kwa Pemba ya leo, sauti ya mti unaokatwa ni zaidi ya kishindo.
Ni kilio cha mazingira kinachoashiria hatari inayozidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Ni sauti inayobeba tahadhari kuhusu mustakabali wa misitu, kilimo, uvuvi na maisha ya maelfu ya wananchi wanaotegemea rasilimali za asili kwa maisha yao ya kila siku.
Kwa miaka mingi, Pemba imejulikana kwa misitu yake ya asili, mashamba ya karafuu na ukanda wake wa bahari wenye utajiri mkubwa wa viumbe hai.
Hata hivyo, mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ongezeko la joto duniani yameanza kuathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya maisha ya wananchi wa kisiwa hicho.
Leo hii, wakulima wanakabiliwa na misimu ya mvua isiyotabirika, wavuvi wanakumbana na mawimbi makubwa na upepo mkali, huku baadhi ya maeneo ya pwani yakishuhudia mmomonyoko wa ardhi unaotishia makazi, mashamba na miundombinu.
Fatma Hamad Kombo, wa Micheweni, anasema hali ya hewa imebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
"Zamani tulijua msimu wa mvua unaanza lini na unaisha lini, sasa mvua zinachelewa au zinanyesha kwa nguvu kiasi cha kuharibu mazao.
Hali hii imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima kwani mavuno hayaridhishi ," anasema.
Naye Amina Bakar mkaazi wa Chake Chake, anasema ongezeko la joto limeathiri hata upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo.
"Kuna vipindi ambavyo visima vinapungua maji tofauti na zamani, hali hii inaonesha kuwa mazingira yanabadilika na tunapaswa kuyatunza zaidi," anasema.
Kwa upande wake Hamad Kidole mvuvi wa Kojani Wilaya ya Wete, anasema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri shughuli za uvuvi.
Anasema zamani hawakuwa na wasiwasi wanapotoka nyumbani kuelekea mavuvini kwani samaki walikuwa wakumwaga ila kwa sasa tokea wanapotoka nyumbani ni hofu Hadi wanaporudi.
"Bahari imebadilika, kuna siku nyingi hatuwezi kwenda kuvua kutokana na upepo mkali na mawimbi makubwa, samaki pia wamepungua tofauti na zamani siku nyingi tunakwenda tukarudi watupu ," anasema.
Kauli yake inaungwa mkono na Juma Haji mkazi wa Mkoani, ambaye anasema wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira ili kuokoa vizazi vijavyo.
"Tukiharibu mazingira leo, watoto wetu hawatakuwa na cha kurithi kesho, kila mmoja wetu ana wajibu wa kulinda misitu, vyanzo vya maji na bahari," anasema.
Kauli za wananchi hao zinaungwa mkono na utafiti uliofanywa mwaka 2023 na Chuo cha Usafirishaji wa Baharini Tanzania (MNMA) katika wilaya za Micheweni, Wete na Chake Chake.
Utafiti huo ulihusisha kaya 361 na kubaini kuwa asilimia 82 ya wananchi waliohojiwa walishuhudia kupungua kwa samaki baharini katika miaka ya karibuni.
Aidha, asilimia 68 walieleza kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo upepo mkali, mawimbi makubwa na mabadiliko yasiyotabirika ya misimu ya mvua.
Athari hizo zimeonekana pia katika sekta ya karafuu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Pemba.
Utafiti uliochapishwa mwaka 2025 kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wa karafuu Pemba ulibaini kuwa asilimia 51.1 ya wakulima walikumbwa na ukavu wa miti ya karafuu.
Asilimia 24.4 walikabiliwa na ongezeko la magonjwa na wadudu waharibifu wa mazao huku asilimia 34.4 wakiripoti changamoto za uotaji wa miche kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa mujibu wa watafiti hao, kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua za uhakika vinaendelea kuhatarisha uzalishaji wa zao la karafuu ambalo kwa muda mrefu limekuwa tegemeo muhimu la uchumi wa Zanzibar.
Kadhalika, utafiti uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Wilaya ya Micheweni umeonesha kuwa katika kipindi cha takribani miaka 30 iliyopita kumekuwa na mabadiliko ya mwenendo wa mvua pamoja na ongezeko la joto.
Wataalamu wanaeleza kuwa hali hiyo imechangia kupungua kwa uzalishaji wa mazao, kuongezeka kwa wadudu waharibifu na changamoto za upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo ya Pemba.
Athari za mabadiliko ya tabianchi hazijaishia katika kilimo na uvuvi pekee maeneo mengi ya pwani Zanzibar yanaendelea kushuhudia mmomonyoko wa fukwe unaotokana na kuongezeka kwa kina cha bahari na nguvu ya mawimbi.
Wataalamu wanaonya kuwa visiwa vidogo kama Zanzibar na Pemba viko katika hatari kubwa ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na mazingira yake ya ukanda wa pwani.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), jamii zinazoishi katika maeneo ya visiwa vidogo na ukanda wa pwani ndizo zinazokabiliwa zaidi na hatari ya mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na kuharibika kwa mifumo ya ikolojia inayotegemewa kwa chakula na kipato.
Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) linaeleza kuwa kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunahitaji uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira, usimamizi endelevu wa rasilimali za asili na elimu kwa wananchi
Mashirika mengine ya kimataifa kama World Wide Fund for Nature (WWF) na International Union for Conservation of Nature (IUCN) nayo yameendelea kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi misitu, mikoko na viumbe hai kama njia ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda maisha ya jamii.
Kutokana na changamoto hizo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuhimiza hatua mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla, amekuwa akisisitiza umuhimu wa usimamizi bora wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili ili kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Naye Kaimu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, amesema ushiriki wa wananchi katika kampeni za upandaji miti, uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi ni msingi muhimu wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Sera ya Mazingira ya mwaka 2013 imetoka muongozo juu ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia mchango wa jamii katika uhifadhi wa mazingira, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu Pemba (CFP), Mbarouk Mussa, anasema changamoto za mabadiliko ya tabianchi haziwezi kutenganishwa na uharibifu wa misitu.
"Misitu ni kinga muhimu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, tunapokata miti bila kuipanda upya tunachangia kuongezeka kwa joto, kupungua kwa mvua na kuharibu makazi ya viumbe hai.
Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika uhifadhi wa misitu," anasema.
Mbarouk anasema juhudi za uhifadhi wa mazingira zimeanza kuleta matokeo chanya ambapo miti (mikoko) inaendelea kupandwa katika maeneo mbalimbali ya Pemba ikiwemo maeneo ya pwani ikiwa ni katika jitihada za kurejesha mazingira yaliyoharibiwa na kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Anasisitiza kuwa mafanikio hayo yataendelea kuwa na maana iwapo wananchi wataendelea kushiriki katika kulinda misitu, mikoko na vyanzo vya maji ambavyo ni msingi wa maisha na maendeleo ya jamii.
Wataalamu wa mazingira Ali Abdi Mohamed kutoka kitengo cha tabianchi Idara ya Mazingira Pemba wanaeleza kuwa misitu ina mchango mkubwa katika kufyonza hewa ya ukaa ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la joto duniani.
Hivyo, upandaji na uhifadhi wa miti ni miongoni mwa njia bora zaidi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kadiri dunia inavyoendelea kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, sauti ya mti unaokatwa inapaswa kuwa mwito wa kuchukua hatua za haraka.
Kwa Pemba, ambako wananchi wengi wanategemea kilimo, uvuvi na misitu kwa maisha yao ya kila siku, kulinda mazingira si suala la hiari bali ni suala la uhai.
Kila mti unaookolewa leo ni ahadi ya mvua za kesho, kila msitu unaohifadhiwa ni kinga dhidi ya ukame, mafuriko na njaa.
Na kila mwananchi anayeshiriki katika uhifadhi wa mazingira anakuwa sehemu ya suluhisho la kuijenga Pemba na Zanzibar yenye ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Bila hatua za pamoja leo, sauti ya mti unaokatwa inaweza kuwa kilio cha kesho, ingawa kwa mshikamano, elimu na uwajibikaji wa kila mmoja, kilio hicho kinaweza kubadilika kuwa sauti ya matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Maamuzi tunayofanya leo ndiyo yatakayoamua kama tutairithisha dunia yenye kijani au jangwa la kesho.
MWISHO
0 Comments