NA HABIBA ZARALI-PEMBA
WAKULIMA wa kilimo msitu shehia ya Kiuyu Minungwini wameanza kuwa na matumaini ya kupata mazao ya chakula ikiwemo ndizi na mananasi kupitia kilimo hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari wa vyombo tofauti huko kijijini kwao kiuyu walisema kilimo hicho ambacho kimo ndani ya mradi wa ‘Zanz Adapt’ tayari mafanikio yake yameanza kuonekana.
Fatma Shaha Faki ni mmoja wa wakulima hao aliyepanda migomba ipatayo 120 alisema tayari baadhi yameanza kuzaa na kupata ndizi kwa chakula.
Alifahamisha kwa hatuwa ya awali mazao hayo anayatumia kwa chakula kwa vile hayajachanaganya kuzaa na kusema kuwa matarajio yake kwa siku za mbele yatazaa kwa wingi na ataweza kuuza na kupata pesa za kujikimu na maisha ya kila siku.
Alisema elimu waliyoipata ya kulima kilimo hicho cha kitaalamu cha kupanda miti mikubwa na midogo katika eneo moja kitaleta manufaa kwa mtu mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla.
Nae Zaituni Shaha Rajab alisema wamejikita katika kilimo hicho wakiwa na nia moja ya kupata mafanikio ambayo sasa wameanza kuyaona.
Akitaja chanagamoto katika kilimo hicho alisema ni pamoja na suala zima la maji,wizi wa mazao na ufungaji wa wanyama na kuwaharibia vipando vyao.
“Ingawa tayari tumeshaanza kula matunda ya kilimo chetu lakini bado tunahitaji kuwezeshwa kupata visima vya maji ili tuweze kumwagilia vipando vyetu”,alisema.
Kwa upande wake Sada Ali Pandu mkulima kiongozi wa kilimo kandaa alisema tayari wameshapanda mikandaa isiyopunguwa 300 jambo linaloleta faraja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akitaja athari za mabadiliko ya tabia nchi ni pamoja na watu kuhama makaazi yao kwa maji kupanda juu, kupotea mazalio ya samaki na kuharibu mashamba ya wakulima.
Fatma Hamad Ali alisema tokea kupata mafunzo yahusuyo mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na mwamko wa jamii kuhusu utunzaji wa mikanadaa.
Kombo Khatib Bakar aliwataka wanaume kijijini hapo kuhakikisha wanawasaidia wanawake na kuwahimiza kutumia fursa zitokanazo na mradi huo ili kutatua chanagamoto zinazowakabili.
Afisa mradi wa Zanzadapt kutoka Tamwa Zanzibar Nafda Hindi Mohamed aliitaka jamii kuwaunga mkono wakulima hao ili malengo ya mradi yaweze kutimia.
Alisema Tamwa inaendelea kutowa elimu mbalimbali kupitia mradi huo ikiwemo umiliki wa ardhi kwa wanawake na kusisitiza mashirikiano katika kila hatua .
Mkakati wa serikali kuhusu kilimo na mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kuelimisha wakulima juu ya kilimo mseto, kukuza mbinu za kilimo zinazoweza kuvumilia mabadiliko ya hali ya hewa kama ukame ama mafuriko .
Kupunguza ukataji wa miti kwa kutoa mbadala wa kuni , kupunguza utowaji wa gesi chafu kutoka kwenye shughuli za kilimo, kuongeza tija bila kuharibu mazingira.
Mradi huo unaolenga kuwanyanyua wanawake kiuongozi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi unaoendeshwa na Tamwa Zanzibar, jumuiya ya hifadhi ya misitu ya jamii Pemba CFP na jumuiya ya kimataifaya hifadhi ya misitu CFI kwa ufadhili wa Serikali ya Canada.
mwisho
0 Comments