MABASI YA MWENDOKASI YASHAMBULIWA JIJINI DAR ES SALAM

Baadhi ya Wakazi wa Jiji waliodai kuchoshwa na kero na kusuasua kwa huduma za Mabasi ya Mwendokasi, wameyashambulia kwa mawe Mabasi ya Mwendokasi pamoja na Vituo vinne vya Mabasi hayo Jijini Dar es salaam.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maaulum ya Dar es salaam Muliro Jumanne kwenye mahojiano na vyombo vya habari, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa vurugu zimetokea katika Vituo vinne vya Mabasi hayo ambavyo ni Gerezani, Magomeni Mapipa, Usalama na Kagera na kuongeza kuwa tayari Polisi wanawahoji Watu kadhaa kutokana na matukio hayo.

““Kuna fujo zilitokea pale Gerezani na ikaja ikatokea Magomeni Mapipa, Usalama na Kagera kuna gari ilichelewa pale Gerezani kuna Watu wakafanya fujo pale kwa kulishambulia, baadae kuna gari lilikuja pale Mapipa likapata hitilafu Abiria wakashuka na baadhi ya Abiria wakachukua mawe wakaharibu lile gari kwenye baadhi ya vioo”  ameeleza Kamanda Muliro.

“Kazi yetu kuhakikisha usalama unaimarika, mpaka sasa kuna Watu tunawahoji ambao inadaiwa walikuwa sehemu ya vurumai, pia baadhi walifanya fujo maeneo ya Kituo cha Polisi cha Usalama na pale Kagera baadhi ya magari yakaharibiwa vioo vyake na baadhi ya Vituo vikapata madhara ya fujo zile” - Muliro.

“Polisi walifika na kudhibiti hali ile maeneo ya Kagera sababu mabasi yalikuwa yanapandisha Ubungo mpaka Kimara, hali ile ilithibitiwa na kusema kweli pamoja na sababu mbalimbali zilizokuwa zinaelezwa lakini suala la kuharibu miundombinu ya usafiri ni kosa kisheria hata ukitoa sababu mbalimbali, maeneo ya Kagera lile kundi tulilazimika kuhakikisha kwamba wanajua Polisi amefika pale wakatawanyika pale wakakimbilia maeneo Mburahati” - ameeleza Kamanda Jumanne Muliro. 

Post a Comment

0 Comments