Aahidi kuendeleza miradi ya maendeleo, kusimamia elimu, afya na ustawi wa jamii kupitia uongozi wa huruma na uwajibikaji
NA-HABIBA ZARALI-PEMBA
Kama ilivyokuwa mwaka 2020, jina la Biharusi Saidi Suleiman linaendelea kutajwa kwa heshima katika vikao vya kisiasa na kijamii ndani ya Jimbo la Wete na Zanzibar kwa ujumla.
Mwanamke huyu mchapakazi na mwenye dira, anayegombea nafasi ya uwakilishi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amejipambanua kama kiongozi wa vitendo si wa maneno.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni humo, Bi. Biharusi aliwaomba wananchi kumpa tena fursa ya kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
“Niliahidi maendeleo, niliyatekeleza na sasa naomba fursa nyingine niendelee kuijenga Wete yetu.
Mwanamke akikabidhiwa dhamana, hutekeleza kwa moyo wa mama kwa upendo na uaminifu.”
Miradi ya Maendeleo Iliyotekelezwa 2020–2025
Katika muhula wake uliopita, Biharusi Saidi Suleiman amefanikiwa kutekeleza miradi kadhaa muhimu jimboni Wete.
Kazi zake zimeshuhudiwa katika sekta za elimu, afya, na ustawi wa jamii.
Skuli ya Tungamaa alisimamia ujenzi wa skuli hiyo mpya kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Bopwe alijenga madarasa matano, akakarabati vyoo 11, na kujenga karo ili kuboresha mazingira ya usafi shuleni.
Kijiji cha Utaaani Kwa ushirikiano na walimu na wananchi, alianzisha darasa la kompyuta kwa lengo la kuwaandaa vijana na maarifa ya kidigitali.
Mkwajuni na kilimahewa aliongoza ujenzi wa kisima cha maji safi kilichosaidia mamia ya wakazi wa eneo hilo.
Skuli ya Jadida alijenga darasa moja la nasari, huku la pili likijengwa kwa ushirikiano na mpango wa TASAF.
Kazi hizi zinathibitisha falsafa yake kwamba “uongozi ni huduma, si heshima.”
Anapewa Sifa kwa Uongozi wa Uwajibikaji
Wakizungumza katika mikutano yake ya kampeni, wananchi wa Wete wamemuelezea Biharusi kama kiongozi asiyeogopa kazi ngumu.
Wengine wameeleza kuwa anawasiliana moja kwa moja na wananchi wake, husikiliza matatizo yao, na mara nyingi hutumia hata rasilimali zake binafsi kusaidia jamii.
Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Jamii ya Zanzibar (2019), viongozi wa umma wanapaswa kuwa na uwajibikaji wa kijamii na uwazi katika matumizi ya rasilimali, Biharusi amekuwa mfano halisi wa utekelezaji wa sera hiyo.
Ushirikiano wa Kijinsia na Wito wa TAMWA
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kupitia tamko lake la mwaka 2025, limewahimiza wananchi kuendelea kuwaamini wanawake viongozi kwa sababu “wanawake ni nguzo ya maadili, uadilifu na maendeleo shirikishi.”
Katika tamko hilo, TAMWA ilisema:
“Wanawake viongozi wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi ni walezi wa jamii na watetezi wa haki.”
Kauli hii inaendana na dhamira ya Biharusi, ambaye alisema wanawake wanapopewa nafasi ya kuongoza, wanatekeleza pale panapohitajika, na si watu wa maneno matupu.
“Nilikuwa nikishirikiana na viongozi wa ngazi zote, lakini mara nyingi nimejifunza kuwa wanawake ni walezi na watekelezaji wazuri. Wanaona maumivu ya jamii kama mama anavyoona uchungu wa mwanawe,” alisema Bi. Biharusi.
Sera na Sheria Zinazounga Mkono Uongozi wa Mwanamke
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Ibara ya 21(1) inamtambua kila raia kuwa na haki ya kushiriki katika uongozi wa umma bila ubaguzi wa kijinsia.
Hivyo, mgombea kama Biharusi anatekeleza haki ya kikatiba ya kuwa sehemu ya maamuzi ya taifa.
Aidha, Sera ya Jinsia Zanzibar (2020) inasisitiza kuwa usawa wa kijinsia katika uongozi ni chachu ya maendeleo endelevu hii inakubaliana pia na Mkataba wa Kimataifa wa CEDAW (1979), unaolenga kuondoa kila aina ya ubaguzi dhidi ya wanawake.
Kwa mujibu wa Sera ya Elimu Zanzibar (2018), miradi ya kielimu inayotekelezwa na viongozi wa ngazi za jamii ni sehemu muhimu ya kukuza elimu jumuishi — jambo ambalo Bi. Biharusi amelifanikisha kwa vitendo.
Anahimiza Ushirikiano na Amani
Biharusi amesisitiza kuwa maendeleo hayatawezekana bila amani na ushirikiano kati ya wananchi, viongozi, na taasisi za serikali.
“Ninaomba wananchi wote wa Wete kudumisha amani kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.
Amani ndiyo urithi bora kwa vizazi vijavyo,” alisema wakati wa mkutano wake wa kampeni.
Kauli hiyo inaendana na Sera ya Usalama wa Taifa (2021) na Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Zanzibar, inayosisitiza wajibu wa vyombo vya ulinzi kulinda raia kwa haki bila kutumia nguvu kupita kiasi.
Kiongozi Mwanamke wa Maendeleo Shirikishi
Bi. Biharusi Saidi Suleiman anaamini kuwa uongozi wa kweli ni ule unaohusisha wananchi.
Amesema miradi yote aliyotekeleza ilianza kwa vichocheo vya maoni ya wananchi wenyewe, kisha ikapewa uhalisia kwa kushirikiana na serikali na wadau kama TASAF, Wizara ya Elimu, na Mamlaka ya Maji.
“Kila mradi ninaouanzisha ni wa wananchi. Mimi ni kiungo tu kati yao na serikali naomba munichague tena ili tuendelee kusukuma gurudumu la maendeleo kwa pamoja,” alihimiza.
“Uongozi wa mwanamke ni baraka. Tunachohitaji ni imani, maadili na ushirikiano,” alisema Wete ni yetu sote tusitupilie mbali kazi nzuri tulizoanza tuwape wanawake nafasi maana wanapoongoza, jamii inasonga mbele,” alihitimisha.
mwisho
0 Comments