Aahidi kuboresha elimu ya skuli na madrasa, kutatua tatizo la maji safi na kuimarisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi
NA-HABIBA ZARALI-PEMBA
Katika harakati za kisiasa visiwani Zanzibar, jina la Khadija Abdullatif Salim limeanza kung’aa kwa kasi kama sauti ya matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Gando, kisiwani Pemba.
Kupitia Chama cha Wananchi (CUF), mgombea huyu wa nafasi ya uwakilishi ameweka bayana dira yake ya mabadiliko kupitia kauli mbiu yenye mvuto “Gando Mpya, Maendeleo kwa Wote.”
Ni mwanamke anayesimamia misingi ya usawa, haki na utumishi kwa wananchi, akiamini kwamba maendeleo hayana jinsia, bali yanahitaji dhamira, uadilifu na uongozi wa haki.
Anataka Kuboresha Elimu ya Skuli na Madrasa
Moja ya nguzo kuu katika sera zake ni kuboresha sekta ya elimu, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu zote mbili skuli na madrasa.
Khadija Abdullatif anaamini kwamba elimu bora ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yoyote.
Anasema kuwa baadhi ya shule katika Jimbo la Gando bado zinakabiliwa na changamoto za walimu wachache, ukosefu wa vifaa vya kufundishia na mazingira duni ya kujifunzia.
“Nataka kuona kila mtoto wa Gando anapata elimu bora ya dunia na dini, ili awe na maarifa na maadili,” alisema wakati wa mkutano wa kampeni katika jimbo la Gando.
Ameahidi kuanzisha mpango wa pamoja kati ya wazazi, walimu, serikali na mashirika ya kijamii kuboresha shule na madrasa, sambamba na kuwasaidia wanafunzi wanaotoka familia zenye kipato cha chini.
Sera hii inakwenda sambamba na Sera ya Elimu ya Zanzibar (2018) inayolenga kutoa elimu jumuishi na yenye ubora kwa watoto wote, bila kujali jinsia au eneo wanaloishi.
Atashughulikia Changamoto ya Maji Safi na Salama
Changamoto ya maji safi na salama imekuwa kero kubwa kwa wakaazi wa Gando, hasa katika maeneo ya Bandani na Fundo.
Mgombea huyo amesema changamoto hii ni kikwazo cha maendeleo na afya bora, hivyo imepewa kipaumbele cha juu katika mpango wake wa maendeleo ya jimbo.
“Maji ni uhai nitaongoza juhudi za kujenga visima virefu, matenki ya kuhifadhia maji na kuboresha mtandao wa mabomba hii ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi,” alisema mgombea huyo.
Kwa mujibu wa Ibara ya 13 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kila raia ana haki ya kupata huduma bora za kijamii kama maji, afya na elimu.
Hivyo, ahadi ya mgombea huyu ni utekelezaji wa haki ya msingi ya wananchi wake.
Aidha, anapanga kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) na wadau wa maendeleo kama UNICEF kuhakikisha Gando inapata maji safi na salama kwa kudumu.
Amani Kabla, Wakati na Baada ya Uchaguzi
Mbali na masuala ya maendeleo, Khadija amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na umoja wakati wa mchakato wa uchaguzi.
“Uchaguzi sio uwanja wa mapambano ni fursa ya kikatiba ya kuchagua viongozi wetu amani ndiyo msingi wa maendeleo,” alisema kwa msisitizo.
Ameziomba taasisi za ulinzi na usalama kuhakikisha wanalinda raia na mali zao kwa mujibu wa sheria, bila kutumia nguvu kupita kiasi.
Kauli yake inalingana na Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Zanzibar, ambayo inawataka maafisa wa usalama kulinda raia na mali zao kwa haki na bila upendeleo.
Pia inaimarisha utekelezaji wa Sera ya Usalama wa Taifa (2021), inayosisitiza kujenga jamii yenye utulivu na kuheshimiana.
Mwanamke Kama Nguvu ya Uongozi
Khadija Abdullatif ni miongoni mwa wanawake wachache wanaoendelea kuvunja vikwazo vya kijamii na kitamaduni kuhusu uongozi.
Anasema kuwa wanawake wanayo nafasi ya msingi katika kujenga taifa, kwani wana uthubutu, maono na uadilifu unaohitajika katika siasa za kisasa.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Ibara ya 21(1), kila raia ana haki ya kushiriki katika siasa, na Sera ya Jinsia Zanzibar (2020) inaweka bayana kuwa ushiriki wa wanawake katika uongozi ni nguzo ya usawa na maendeleo.
Kwa upande wa dini, Uislamu unamruhusu mwanamke kushika madaraka, kama ilivyokuwa kwa Bi Khadija bint Khuwaylid (RA), mke wa Mtume (SAW), aliyekuwa kiongozi wa biashara na mfano wa hekima.
Vivyo hivyo, Ukristo unasema katika Wagalatia 3:28 kwamba “hakuna mwanaume wala mwanamke, nyote mmekuwa kitu kimoja katika Kristo Yesu.”
“Dini zote mbili zinakubali mwanamke kuwa kiongozi. Kinachohitajika ni uadilifu, busara na uaminifu,” aliongeza mgombea huyo.
Kauli Mbiu: “Gando Mpya, Maendeleo kwa Wote”
Kauli hii ni wito wa mabadiliko chanya. Inalenga kujenga Gando yenye maendeleo jumuishi, usawa wa kijinsia na huduma bora kwa wananchi wote.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar 2020–2050 (ZADEP), ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni nyenzo muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu.
Khadija anasema anataka kuwa “daraja la kuunganisha wananchi na serikali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.”
Uongozi Wenye Maadili na Dira ya Kitaifa
Khadija Abdullatif anajitambulisha kama mwanamke wa maadili, asiyeamini siasa za lawama, bali anataka siasa za hoja na maendeleo.
Ameahidi kuwa mtetezi wa haki za wananchi, hasa wanawake na vijana, ndani ya Baraza la Wawakilishi, endapo wananchi watampa dhamana hiyo.
“Gando inahitaji mabadiliko, na mabadiliko hayo yatakuja kupitia umoja, elimu bora, huduma za maji safi na amani ya kudumu,” anasisitiza.
Kwa sera zake, msimamo wake wa kisheria na misingi ya dini, Khadija Abdullatif Salim anaonekana kuwa kiongozi mwanamke, anayejua anachokisimamia.
mwisho
0 Comments