Husna Mohamed Abdallah: Kiongozi Mwanamke Mwenye Dira, Anayeamini Katika Haki, Maslahi na Maendeleo kwa Watanzania Wote



Mgombea mwenza wa CUF aahidi mageuzi katika maslahi ya watumishi wa umma na kuimarisha utawala bora unaoweka mwananchi mbele

NA-HABIBA ZARALI-PEMBA
Katika uwanja wa siasa za Tanzania, jina la Husna Mohamed Abdallah limekuwa gumzo jipya linalowasha moto wa matumaini, hususan kwa wanawake na vijana wanaotamani kuona mabadiliko ya kweli katika uongozi wa taifa.

Akiwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), Husna amejipambanua kama sauti ya mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutawala, akibeba ajenda mahsusi ya kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma na kuhakikisha serikali inatoa huduma bora kwa wananchi.

 “Mtumishi wa umma akiwa na maslahi bora, jamii nzima inanufaika bila chama cha CUF, hakuna maendeleo ya kweli Zanzibar,” alisema kwa msisitizo katika moja ya mikutano yake ya kampeni.
Ajenda Kuu: Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Umma

Katika sera zake, Husna Mohamed Abdallah ameweka kipaumbele kwenye mageuzi ya mfumo wa ajira na mishahara ya watumishi wa umma. 

Ameahidi kuwa chama chake kitatekeleza kwa vitendo mageuzi ya kiutawala yatakayorejesha imani ya wananchi kwa serikali.

 “CUF itahakikisha tunaboresha maslahi ya watumishi wa umma tutapitia upya mfumo wa mishahara, kuondoa kikokotoo kisicholipa haki, na kuweka sheria zitakazomlinda kila mtumishi wa umma dhidi ya dhuluma kazini,” alisema.

Kwa mujibu wa Sera ya Utumishi wa Umma ya Tanzania (2008), mtumishi wa umma ni mhimili wa utekelezaji wa maendeleo ya taifa. 

Hata hivyo, changamoto za mishahara midogo, kuchelewa kupandishwa madaraja na ukosefu wa stahiki zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu.

Husna anaamini kuwa kwa kurekebisha maslahi na mazingira ya kazi, watumishi watafanya kazi kwa ari, tija na uadilifu, jambo litakalowezesha wananchi kupata huduma bora.

Sheria na Uongozi wa Haki

Mgombea huyo mwenza anasema mageuzi haya yataambatana na maboresho ya kisheria yatakayohakikisha watumishi wa umma wanatekeleza wajibu wao kwa uadilifu bila woga wala upendeleo.

“Tutatengeneza sheria zenye meno, zinazowalazimisha viongozi kuwahudumia wananchi, Serikali lazima iwe ya uwajibikaji, si ya vitisho,” alisema.

Kauli hii inaendana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Ibara ya 8(1)(c) na 9(f), zinazoweka wajibu wa serikali kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa uwazi na uadilifu kwa maslahi ya wananchi.

Aidha, Katiba ya Zanzibar ya 1984 inasisitiza haki ya wananchi kupata huduma bora na kushirikishwa katika maamuzi yanayohusu maisha yao.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (1981) na Mkataba wa CEDAW (1979), nchi wanachama zinatakiwa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi na kufanya maamuzi yanayogusa maslahi ya jamii.


Uongozi wa Mwanamke: Nguzo ya Maendeleo Endelevu

Husna Mohamed Abdallah ni mfano wa kizazi kipya cha wanawake viongozi wanaoamini kuwa maendeleo yanahitaji ushiriki wa jinsia zote mbili.

Kwa mtazamo wake, wanawake ni walezi wa jamii, wahamasishaji wa amani, na watekelezaji wazuri wa mipango ya maendeleo.

Anasema serikali yenye usawa wa kijinsia huchochea tija na kupunguza rushwa.

 “Wanawake tunajali, tunasikiliza, na tunatekeleza tukipewa nafasi ya kuongoza, tunabadilisha maisha ya watu kwa matendo, si kwa maneno,” alisema Husna.

Kauli yake inaungwa mkono na Sera ya Jinsia Tanzania (2000) na Sera ya Jinsia Zanzibar (2020) ambazo zinasisitiza ushirikishwaji wa wanawake katika uongozi kama chachu ya maendeleo endelevu.

Mageuzi Kupitia CUF: Serikali ya Watu kwa Ajili ya Watu

Chama Cha Wananchi (CUF), kupitia sera zake kuu za haki, usawa na uwajibikaji, kimekuwa mstari wa mbele kupigania mfumo wa utawala unaoweka wananchi mbele ya kila kitu.

Husna Mohamed Abdallah anasema sera ya CUF ni kuondoa vikwazo vya kiutawala vinavyowazuia watumishi kutoa huduma bora, kwa kuondoa ukiritimba, urasimu na vitisho kazini.

 “CUF tumejipanga kurejesha thamani ya utumishi wa umma mtumishi atapata mishahara bora, posho stahiki, bima ya afya yenye hadhi, na mazingira bora ya kazi,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Sera ya Ajira ya Taifa (2008), malengo ya serikali ni kuhakikisha ajira yenye staha na tija kwa wote.

Mageuzi anayoyapendekeza Husna yanaendana na sera hiyo na ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs 2030), hususan lengo namba 8  “Ajira zenye hadhi na ukuaji wa uchumi.”


Dini na Maadili Katika Uongozi

Husna Mohamed Abdallah ni kiongozi anayeamini katika maadili ya kidini anaona uongozi kama dhamana, si fursa ya kujinufaisha.

Kwa mujibu wa Uislamu, Mtume Muhammad (SAW) alisema:

 “Kiongozi ni mchungaji wa watu wake, na ataulizwa kuhusu uchungaji wake.”

Halikadhalika, maandiko ya Kikristo (Luka 22:26) yanasema, “Awa mkubwa kwenu na awe kama mtumishi.”

Kwa misingi hii, Husna anasisitiza kuwa serikali inayomtegemea Mungu na kuheshimu maadili ndiyo inayoweza kuleta maendeleo ya kweli.

Kauli Mbiu: “CUF kwa Maendeleo, Haki na Maslahi ya Wote”

Kauli mbiu hii inaelezea falsafa ya Husna Mohamed Abdallah  kwamba chama cha CUF kinalenga kuleta mageuzi ya kweli kupitia uongozi wa haki na uadilifu.

Kwa mujibu wake, maendeleo hayataletwa na ahadi tupu bali na utekelezaji wa sera zenye kutanguliza utu wa mwanadamu.
Anawataka Watanzania wa Bara na Zanzibar kuamini kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa ufanisi sawa au zaidi.

 “Serikali ya CUF itahakikisha kila mwananchi ananufaika na rasilimali za taifa tutaboresha utumishi wa umma na kuondoa mifumo kandamizi inayozuia maendeleo,” alisisitiza.

Msimamo Wake Kuhusu Zanzibar na Muungano

Husna anasema bila CUF, hakuna maendeleo ya kweli Zanzibar, kwani chama hicho ndicho kinachobeba ajenda ya usawa wa kiuchumi na kijamii ndani ya Muungano.

Ameeleza kuwa watumishi wa umma wa Zanzibar watapata nafasi sawa na wale wa Bara, na serikali ya CUF itahakikisha rasilimali zinagawanywa kwa uwiano unaostahili kwa mujibu wa Katiba ya Muungano (1977).

 “CUF inaheshimu Muungano, lakini tunataka Muungano wenye usawa na manufaa kwa pande zote mbili,” alisisitiza.

 Mwanamke Mwenye Dira, Msimamo na Maono ya Kitaifa

Husna Mohamed Abdallah ni mfano wa mwanamke anayechanganya busara, elimu na ujasiri katika siasa. 

Anaamini kuwa mageuzi ya kweli yanahitaji ujasiri wa kuchukua hatua na dhamira safi ya kulitumikia taifa.

Kwa sera zake, msimamo wake wa kisheria na wito wa kijinsia, anabaki kuwa kielelezo cha kizazi kipya cha wanawake viongozi wanaoamini kwamba uongozi wa mwanamke si upendeleo, bali ni haki na hitaji la maendeleo endelevu.

mwisho

Post a Comment

0 Comments