NA-HABIBA ZARALI-PEMBA
Katika harakati za kisiasa za visiwa vya Zanzibar, jina la Yumna Ahmed Khalid limeibuka kwa kishindo kama sauti ya matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Chambani kupitia Chama cha ADA TADEA.
Ni mwanamke kijana, jasiri na mwenye maono mapana, aliyeamua kugombea nafasi ya uwakilishi jimbo la Chambani huku akiwakilisha kizazi kipya cha viongozi wanawake wanaoamini katika misingi ya usawa, maendeleo na uadilifu.
Kupitia sera zake zenye kujikita katika elimu, ajira na afya, Yumna ameonesha dhamira ya kweli ya kuwa daraja la wananchi wa Chambani kuvuka changamoto za kimaendeleo na kufikia mustakabali bora.
Dira ya Kiongozi Mwanamke: Kujenga Jimbo lenye Elimu Bora na Afya Imara
Katika mikutano yake ya kampeni, Yumna amesisitiza kwamba changamoto za elimu, ajira na afya ni miongoni mwa vikwazo vikubwa vinavyozurura katika maisha ya wananchi wa Chambani.
Anaeleza kuwa, ukosefu wa miundombinu ya kielimu bora, uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia umekuwa ukichangia kushuka kwa viwango vya ufaulu, hasa katika shule za msingi na sekondari za vijijini.
“Elimu ndiyo ufunguo wa maendeleo bila elimu bora, hatuwezi kupata wataalamu, viongozi wa kesho wala uchumi imara,” anasema kwa msisitizo.
Katika mpango wake wa maendeleo wa jimbo hilo, Yumna ameahidi kuanzisha mfuko maalum wa maendeleo ya elimu utakaoshirikisha wazazi, walimu na serikali za mitaa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Pia anapanga kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuwezesha vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali, hatua itakayopunguza tatizo la ajira na utegemezi.
Ukarabati wa Kituo cha Afya na Upatikanaji wa Vifaa Tiba
Sekta ya afya imepewa kipaumbele maalum katika ajenda ya Yumna anasema wazi kwamba ana mpango wa kufanya ukarabati wa kituo cha afya cha Chambani, kuboresha majengo yake, na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na dawa muhimu kwa wagonjwa.
Anaamini kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya jamii, na mwananchi mwenye afya njema ana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa sera za Chama cha ADA TADEA, afya bora ni haki ya msingi ya binadamu, kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inayosema “Kila mtu ana haki ya kuishi, kupata huduma za afya na kulindwa maisha yake.”
Kwa msingi huo, Yumna anasimama kama mtetezi wa utekelezaji wa haki hii ya kikatiba kwa vitendo, si kwa maneno pekee.
Ajira kwa Vijana: Kipaumbele cha Kimkakati
Tatizo la ajira, hususan kwa vijana, limekuwa changamoto kubwa katika Zanzibar nzima Yumna anaamini kuwa tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa maneno ya kisiasa pekee bali kwa mipango endelevu inayozingatia sera za kitaifa na mkataba wa ajira unaozingatia usawa wa kijinsia.
Anaeleza kuwa atashirikiana na taasisi za serikali, sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo (internship) na miradi midogo ya ujasiriamali kwa vijana wa Chambani.
Pia anapanga kuhamasisha wanawake na vijana kutumia fursa za mikopo midogo (microfinance) zinazotolewa na taasisi za kifedha na mashirika ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Sera ya Ajira ya Zanzibar (2018), kila jimbo linapaswa kuweka mikakati ya ndani ya kukuza ajira kupitia sekta za kilimo, uvuvi, biashara ndogo na utalii Yumna ameahidi kuwa ataisimamia sera hiyo ipasavyo ndani ya jimbo lake.
Misingi ya Kisheria na Kidini: Mwanamke na Uongozi
Yumna Ahmed Khalid ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi, akiamini kwamba wanawake wana haki ya kugombea na kushika nafasi za uongozi kwa mujibu wa sheria, sera na hata mafundisho ya dini.
Kisheria, Katiba ya Zanzibar Ibara ya 21(1) inatoa haki kwa kila raia kushiriki katika shughuli za kisiasa, bila kujali jinsia, rangi au dini.
Hii inaendana pia na Mkataba wa Kimataifa wa kutokomeza ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) ambao Zanzibar ni sehemu yake.
Mkataba huu unahimiza nchi wanachama kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kipengele cha kidini pia hakina pingamizi. Katika Uislamu, tunajifunza kutoka kwa wanawake mashuhuri kama Bi Aisha (RA) na Bi Khadija (RA), waliokuwa viongozi na washauri wa Mtume (SAW).
Hii ni ishara kwamba dini haiwakatazi wanawake kushiriki katika uongozi, mradi wanazingatia maadili na uadilifu.
Vilevile, Ukristo unasisitiza usawa wa wanadamu wote mbele za Mungu, kama inavyosema katika Wagalatia 3:28 “Hakuna mwanaume wala mwanamke; nyote mmekuwa kitu kimoja katika Kristo Yesu.”
Kwa msingi huo, Yumna anasimama kama kielelezo cha utekelezaji wa haki hizi kwamba mwanamke anaweza kuwa kiongozi imara, mwenye maono na ufanisi, bila kuvunja misingi ya dini wala mila.
Kuwa Daraja la Kuvuuka Changamoto
Kwa maneno yake mwenyewe, Yumna anasema “Nataka kuwa daraja la wananchi wa Chambani kuvuka kutoka changamoto za elimu duni, ukosefu wa ajira na huduma hafifu za afya kuelekea jamii yenye matumaini, fursa na maendeleo ya kweli.”
Kauli hii imebeba uzito mkubwa wa kiimani, kimaadili na kisera ni wito wa umoja, ushirikiano na uwajibikaji.
Kwa kuzingatia malengo yake, msimamo wake wa kiitikadi, na dhamira ya kweli ya kutumikia wananchi, Yumna Ahmed Khalid anaonekana kuwa miongoni mwa viongozi wanawake wa kizazi kipya wanaoweza kuleta mageuzi ya kimaendeleo ndani ya Zanzibar.
Mwanamke Kama Nguvu ya Mabadiliko kupitia sera, sheria na misingi ya dini, hakuna kizuizi kwa mwanamke kushika madaraka au kuongoza jamii.
Kinyume chake, wanawake kama Yumna ni alama ya mabadiliko na maendeleo uongozi wake unatarajiwa kuwa chachu ya uwajibikaji, ushirikishwaji na ustawi wa wananchi wa Chambani.
Amabae amejipambanua si tu kama mgombea wa ADA TADEA, bali kama nguzo ya matumaini kwa mustakabali wa Jimbo la Chambani na Zanzibar kwa ujumla.
mwisho
0 Comments