Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameendelea na mfululizo wa vikao vyake na waangalizi wa uchaguzi kutoka jumuiya mbalimbali za kimataifa wanaowasili nchini kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Mapema leo, tarehe 27 Oktoba 2025, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inayoongozwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Malawi, Mhe. Richard Msowoya.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa hali ya amani na utulivu iliyopo nchini, hususan katika kipindi chote cha kampeni, inaonesha taswira njema ya kufanyika kwa uchaguzi huru, wazi na wa haki.
Wakati huohuo, Rais Dkt. Mwinyi amekutana pia na waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiongozwa na Makamu wa Rais Mstaafu wa Uganda, Mhe. Specioza Kazibwe.
Aidha, timu nyingine ya waangalizi wa uchaguzi kutoka Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), ikiongozwa na Rais Mstaafu wa Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye, imekutana na Rais Dkt. Mwinyi Ikulu Zanzibar.
0 Comments