MITUNGI YA GESI INAVYOKUWA SILAHA YA KIJANI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI



HABIBA ZARALI-PEMBA

Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa changamoto kubwa duniani, na Zanzibar ikiwa ni  kisiwa, kinabeba mzigo mkubwa wa athari zake ikiwemo mmomonyoko wa fukwe, mabadiliko ya mvua na kuongezeka kwa joto.

Katika mazingira haya, matumizi ya mitungi ya gesi kama nishati safi ya kupikia yameibuka kuwa suluhisho muhimu linalosaidia kupunguza ukataji miti, kulinda afya za wananchi na kupunguza uzalishaji wa gesi joto.
GESI NA MAPINDUZI YA NISHATI SAFI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda mazingira.

Serikali hiyo imeeleza dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati salama, nafuu na endelevu ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa unaochangia uharibifu wa misitu.

USHIRIKI WA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS

Katika utekelezaji wa sera hizo, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa mstari wa mbele katika kampeni za mazingira na nishati safi.

Afisa Mdhamini wa Ofisi hiyo, Ahmed Abubakar Mohamed, amekuwa akishiriki katika shughuli za uhamasishaji wa matumizi ya gesi na ugawaji wa mitungi kwa baadhi ya jamii, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nishati safi na uhifadhi wa mazingira.
ATHARI ZA TABIANCHI ZANZIBAR

Wataalamu wa mazingira wanasema Zanzibar inaendelea kukumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kupanda kwa kina cha bahari, kupungua kwa rutuba ya udongo na kuathirika kwa sekta za kilimo na uvuvi.

Misitu inaendelea kuwa nguzo muhimu ya mazingira, lakini matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakipunguza uoto wa asili, hali inayoongeza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

GESI NA MAISHA YA WANANCHI

Katika maeneo mbalimbali ya Pemba na Unguja, wananchi wanaeleza jinsi matumizi ya gesi yalivyobadilisha maisha yao.


 Fatma Juma wa Mkoani anasema "awali nilikuwa natumia muda mwingi jikoni kutokana na mkaa kuchelewa kuwaka sasa napika haraka na hakuna moshi unaosumbua familia yangu.”

 Mwanahija Suleiman wa Chake Chake anasema moshi wa mkaa ulikuwa unawaathiri sana hasa katika afya ya watoto .
 
"Mimi saivi napikia gesi pekee mkaa sikutaki maana wanicheleweshavhaswa"anasema.

Bi. Halima Omar wa Micheweni anasema gesi imemsaidia kiuchumi inamsaidia kupika kwa urahisi.
“Nina muda zaidi wa biashara yangu badala ya kutumia muda kutafuta kuni.” anasema.

Rahma Juma wa chokocho anasema elimu ya mazingira imebadilisha mtazamo wa jamii ingawa hali za wengi ni za umaskini ila wanatumua .

“Sasa watu wanaelewa kuwa gesi ni nafuu kwa muda mrefu na ni salama ingawa gharama ni kubwa Kwa wanyonge.” anasema

Ali Mohammed wa Machomane Chake Chake anasema "Gesi imerahisisha maisha ya familia yangu na kupunguza matumizi ya mkaa.”

Abdallah Mohamed wa Kojani anaeleza
“Kila mti unaookolewa ni mchango kwa mazingira ya kesho watu wasiikate” 

 Hamad Suleiman wa Mkoani anasisitiza anasema Gesi ni sehemu ya suluhisho la kulinda mazingira na afya.

Idara ya Mazingira Pemba na wadau
Idara ya Mazingira Pemba imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuhifadhi mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.

Pia mashirika ya kimataifa kama United Nations Development Programme, United Nations Environment Programme, Green Climate Fund na Global Environment Facility yamekuwa yakisaidia miradi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira Zanzibar.

SERA, SHERIA, NA MIKAKATI

Sera za nishati na mazingira Zanzibar zimeweka mkazo katika kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuongeza matumizi ya nishati safi na kulinda misitu.

Mikakati hiyo inalenga kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira.

Hitimisho

Wataalamu wa mazingira wanasema mabadiliko ya tabianchi hayawezi kupigwa vita kwa sera pekee bila ushiriki wa wananchi.

Mtungi wa gesi, licha ya kuwa kifaa kidogo cha jikoni, umeibuka kuwa silaha muhimu ya kijani inayosaidia kulinda misitu, kuboresha afya na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa ushirikiano wa serikali, viongozi, taasisi na wananchi, Zanzibar inaweza kuwa mfano wa mafanikio ya nishati safi barani Afrika.

Katika vita hii, kila mtungi wa gesi unaotumika ni hatua moja mbele kuelekea Zanzibar ya kijani na endelevu.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments