NA-ARAFA MAKAME PEMBA.
Zaidi ya shilingi bilioni 127 zimetumika kujengea miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kusini Pemba, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, katika hafla ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru uliofanyika Wingwi uwanja wa mpira Njuguni, wilaya ya Micheweni, wakati akikabidhi Mwenge huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, leo tarehe 4 aprili 2026.
Mkuu huyo ameeleza kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mkoa wa kusini Pemba zilifikia vijiji 40, ambapo vijiji 13 ni vya Chake Chake na 27 kutoka Mkoani, nakukimbizwa kwa umbali wa kilomita 101.9.
Aidha, jumla ya miradi 11 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 127.6 ilihusishwa, ambapo asilimia 99.9 ya fedha hizo zilitolewa na Serikali Kuu na kiasi kidogo kikitokana na nguvu za wananchi.
Katika utekelezaji wake, miradi mitano iliwekewa mawe ya msingi, miwili ilizinduliwa rasmi na minne kukaguliwa, hatua inayoonesha kasi ya maendeleo na usimamizi mzuri wa miradi ya umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatibu Yahya, ameahidi kuukimbiza Mwenge katika wilaya ya Micheweni na Wete zenye jumla ya shehia 38, ambapo miradi 14 itazinduliwa, kuwekwa mawe ya msingi na mengine kukaguliwa.
Aidha, amesema ifikapo Aprili 6, 2026 ameahidi kuukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Mjini Magharibi ukiwa salama huku akihimiza wananchi kudumisha amani, umoja na mshikamano ikiwa chini ya kauli mbiu isemayo, “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.
Mwisho.
0 Comments