Leo Afrika inasimama kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Siku ya kukumbuka damu ya watoto wa Soweto 1976. Siku ya kuuliza, Tuko wapi sasa miaka 50 baadaye?
Jibu ni hili, Mtoto wa Afrika bado anapigania haki ya msingi. Mwaka huu 2026, AU imetuita tuzungumzie MAJI, USAFI NA USAFI WA MAZINGIRA KWA KILA MTOTO.
Kwa sababu ukweli ni mgumu, Mtoto asiye na maji safi shuleni, huacha kusoma. Mtoto bila choo salama, anaibiwa utu wake. Mtoto aliyechafuka na magonjwa, ndoto zake zinakufa kimya kimya.
Viongozi wetu wanasema nini leo?
1. Mhe. Évariste Ndayishimiye, Mwenyekiti wa AU:
“Mtoto wa Kiafrika asiyepata elimu leo ni sehemu ya mustakabali wa Afrika ambayo tunaiacha kesho. Hatuwezi kuijenga kesho bila kumlinda mtoto leo.”
2. Nelson Mandela:
“Hakuna uwazi zaidi wa nafsi ya jamii kuliko jinsi inavyowatendea watoto wake”. Zanzibar yetu, tunaipima vipi nafsi yetu?
3. Dr. Benyam Dawit Mezmur, ACERWC:
“Kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wote ni wajibu wa haki za binadamu”. Ukosefu wa maji ni ukatili. Kunyima mtoto choo shuleni ni ukatili.
4. Kamati ya Wataalamu wa Haki za Mtoto wa AU - ACERWC
Tema ya 2026 inatukumbusha wajibu wetu chini ya Mkataba wa Haki za Mtoto wa Afrika, Ibara ya 14 “Kuhakikisha upatikanaji wa maji salama na usafi”
Na sauti kutoka nchi yetu Tanzania?
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo akiadhimisha na wajukuu zake Ikulu amesema wazi:
“Serikali, familia na jamii tushirikiane kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yenye maadili mema. Usalama wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, siyo mzazi tu. Tuwapatie elimu na historia za kuwahimiza uzalendo tangu wadogo.”
Kauli ya Mama Samia inakamilisha wito wa AU: Mtoto salama, Mtoto mwenye maadili Mtoto mzalendo ni Mustakabali imara wa Afrika.
Na nani anasimama na watoto hapa Zanzibar?
Napiga saluti na kusema ASANTE KUBWA kwa
1. TAMWA Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania - TAMWA -ZANZ, ambao ni miongoni mwa sauti ya mtoto asiyesikika. Ni kalamu inayovunja ukimya wa ukatili.
2. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sera na mipango ya kulinda ustawi wa mtoto.
3. Walimu, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia na kila mzazi anayechagua kumlea mtoto kwa upendo badala ya fimbo.
Ndugu zangu, AU mwaka huu imesema wazi “Watoto wetu si walengwa wa mabadiliko tu bali ni waendeshaji wa mabadiliko ya Afrika”
Basi tusimame. Kila choo tunachojenga shuleni ni darasa. Kila bomba la maji tunalofungua ni wino wa kalamu ya mtoto. Kila mtoto tunayemlinda leo, ni kiongozi tunayempa kesho.
Tusinyamaze. Mtoto akilia kwa njaa ya maji, Afrika nzima inalia.
💧Maji ni haki. Mtoto ni hazina. Kesho ni wetu.
0 Comments