Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameanza kujadili na kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya Shilingi trilioni 8.5 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil.
Majadiliano hayo yanafanyika katika Mkutano wa Tatu, Kikao cha 32 cha Baraza la 11 la Wawakilishi, ambapo wajumbe 11 walipata fursa ya kuchangia na kutoa ushauri kuhusu bajeti hiyo. Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Mhe. Ali Suleiman Ameir (Mrembo), aliwasilisha maoni na mapendekezo ya Kamati hiyo mbele ya Baraza katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar.
Mjumbe wa kwanza kuchangia mjadala huo alikuwa Mhe. Hussein Mohamed Makungu, Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni (CCM), ambaye alieleza kuwa Bajeti Kuu ya mwaka 2026/2027 inatekelezeka kwa asilimia 100 kutokana na kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, hatua ambayo itawezesha Serikali kupata rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuchochea maendeleo ya Zanzibar.
Mhe. Makungu alisisitiza kuwa mafanikio hayo yanatokana na mageuzi yanayoendelea kufanywa na Serikali pamoja na maono ya maendeleo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambayo yameweka mazingira bora ya kukuza uchumi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali.
0 Comments