KATIKA KUKUZA MAENDELEO YA KIELIMU WAZAZI WATAKIWA KUWA NA MASHIRIKIANO

Mratibu wa Idara ya Elimu Sekondari, Bi. Tarehe Khamis Hamad amewataka wazazi, walezi na wanafunzi kuongeza mashirikiano ya karibu na Wizara ya Elimu pamoja na Serikali, ili kuendeleza na kukuza mafanikio makubwa yanayopatikana katika sekta ya elimu.
​Bi. Tarehe ametoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi kompyuta mpakato (Laptop) kwa wanafunzi waliofaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza (Division One) katika mitihani yao ya kitaifa, kwa skuli za Serikali na zile za Binafsi.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu, iliyopo Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

​Mratibu huyo amebainisha kuwa motisha hiyo ya utolewaji wa kompyuta hizo imekuwa chachu kubwa inayowahamasisha wanafunzi kujisomea kwa bidii. 

Aliongeza kuwa, hamasa hiyo imeonekana wazi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ufaulu wa daraja la kwanza kila mwaka.

​Ili kuongeza hamasa zaidi maskulini, Mratibu huyo amewaagiza Wakuu wa Skuli zote zilizofaidika kuhakikisha wanazigawa kompyuta hizo mbele ya wanafunzi wenzao. 
Hatua hiyo inalenga kuamsha ari ya ushindani wa kitaaluma miongoni mwa wanafunzi wanaondelea na masomo ili nao waweze  kuongeza juhudi.

​Katika awamu hii, jumla ya kompyuta mpakato (Laptop) 890 zimekabidhiwa kwa skuli 42, zikiwa ni zawadi maalum kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne (Form 4) na Kidato cha Sita (Form 6) waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kwa miaka tofauti kuanzia mwaka 2023 hadi 2025

Post a Comment

0 Comments